YANGA imemalizana na washambuliaji wawili hadi sasa lakini kama unadhani wamemaliza basi unakosea kwani kocha wao Nasreddine Nabi ametangaza kuwa mashine nyingine lazima ije tena kule mbele.
Yanga imemalizana na mshambuliaji Stephan Aziz KI ambaye hata kabla ya klabu hiyo haijathibitisha Mwanaspoti lilikuwa na uhakika na staa mwingine ni Lazarous Kambole ambaye naye anakuja msimu ujao.
Nabi aliliambia Mwanaspoti kuwa amehakikishiwa na mabosi wa klabu hiyo kuwa atakuwa na KI na Kambole, lakini bado akatamka kwamba anataka mashine nyingine ya mabao na anafikiria kuongeza mshambuliaji mwingine bora zaidi mbali na hao wawili ambaye atakuja kupambana na Fiston Mayele.
“Ndiyo nimeambiwa hao wachezaji wawili tutakuwa nao msimu ujao (KI na Kambole). Ni wachezaji bora sana, klabu kubwa kama hii ni fahari kuwa nao. Unajua najivunia kufanya kazi na wenye nguvu kama Injinia (Hersi Said) lakini nimemwambia bado nafikiria kuhitaji mtu mwingine zaidi,” alisema Nabi.
“Nitahitaji mshambuliaji mwingine, kuna aina ya mtu bora zaidi namtafuta sitaki kuyumba hata kidogo msimu ujao. Tunakwenda kwenye mashindano makubwa huko lazima uwe na watu wasio na mashaka angalau watatu, wapo ambao wataanza kwenye mechi na wengine kusubiri.
0 Comments