Kikosi cha Yanga
UONGOZI wa kikosi cha Yanga, umeweka wazi kuwa wamejiwekea malengo makubwa ya kuhakikisha msimu ujao, angalau wanacheza hatua ya makundi ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

 

Yanga juzi Jumatano usiku waliibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Coastal Union na kufanikiwa rasmi kutangazwa kuwa mabingwa wapya wa Ligi Kuu na kuandika rekodi ya kushinda ubingwa huo kwa mara ya 28.

 

Kwa kushinda ubingwa huo sasa Yanga inakuwa timu ya kwanza kutoka Tanzania kukata tiketi ya moja kwa moja kuiwakilisha nchi katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao.



Yanga na Simba zote zitashiriki katika mashindano ya CAF msimu ujao


Akizungumza na Championi Ijumaa, Msemaji wa Klabu ya Yanga, Haji Manara kuhusu malengo yao katika michuano hiyo msimu ujao alisema: “Tunashukuru kwa kufanikisha lengo letu mama la kushinda ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu, ni wazi halikuwa jambo rahisi kumaliza ukame huu wa misimu minne, hivyo uongozi na wachezaji wanastahili pongezi kwa kazi kubwa.”


 Ubingwa huu una maana kuwa tumefanikiwa kukata tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa msimu ujao, msimu uliopita tulitolewa hatua ya awali lakini msimu huu mpango wetu ni kuhakikisha tunafika angalau hatua ya makundi.”